Vyama vya siasa vimesema hatua ya CCM kujivua gamba haitasaidia kukijenga chama hicho iwapo viongozi wapya wa chama hicho wataendelea kuwa na tabia na hulka za zamani.
Wengine wamemshauri Rais Jakaya Kikwete avunje pia Baraza la Mawaziri, kwani huko ndiko kwenye udhaifu mkubwa wa kiutendaji kuliko kwenye chama.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema litakuwa jambo jema kama CCM imejivua gamba kwa ajili ya kuleta mabadiliko na si kuwa kizingiti cha mabadiliko.
Alisema walichofanya CCM ni jambo la kawaida kila baada ya uchaguzi vyama vimekuwa vikikaa na kuangalia upungufu uliojitokeza na kisha kufanya mabadiliko kujiimarisha.
Profesa Lipumba alisema CCM imekaa madarakani miaka 50, hivyo ni dhahiri inahitaji kufanya mabadiliko makubwa kwa kuwa hivi sasa imepoteza dira na mwelekeo kutokana na kushindwa kutatua kero za wananchi.
Alisema kujivua kwake gamba kusaidie kuleta tume huru ya uchaguzi na kuwezesha mabadiliko ya kuanzishwa kwa katiba mpya.
“Kujivua gamba kwa CCM kutakuwa kuzuri kama watawezesha kufanyika kwa mabadiliko. Ila kama wanajivua gamba kwa ajili ya kuzuia mabadiliko watajiweka pabaya, watu wanataka mabadiliko,” alisema.
Mwenyekiti wa APPT Maendeleo, Peter Mziray, alisema CCM imebaini kuwa kuna ushindani mkubwa wa kisiasa na ndiyo sababu imeaanza kupapatika.
Alisema kinachokiumiza chama hicho, ni ufisadi kama walivyokiri wenyewe na kwa kuwa mafisadi wengi wanatoka chama hicho lazima wajisafishe kama wanataka wananchi wawaamini.
Aliongeza kuwa CCM lazima ikubali kuwa imechoka na kuzeeka na haijaja na ajenda mpya ya kuwashawishi Watanzania kuendelea kuwaamini na haiwezi tena kutawala nchi.
Alisema iwapo CCM itajichanganya na kuteua Katibu Mkuu asiye mwanasiasa itakuwa inajichimbia kaburi kwani kwa hali ilivyofikia chama hicho hakirekebishiki tena.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, alisema CCM kujivua gamba ni sawa na janja ya nyani kwa kuwa nyoka ni yule yule na Watanzania wasitarajie mabadiliko makubwa.
Alisema serikali ya CCM inapaswa kuamka na kuhakikisha inaondoa pengo kati ya maskini na matajiri kwa kuwa limekuwa kubwa na kusababisha umaskini kuzidi kuongezeka.
Mbatia alisema CCM haina itikadi hadi sasa kwani ujamaa waliokuwa wakiuhubiri zamani walishautelekeza na kukumbatia mafisadi, ambao ndio wameifikisha Tanzania katika lindi la umaskini.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisema kuvunjwa kwa sekretarieti ya CCM na CC na Makamba hakutasaidia sana kwa kuwa baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi waliotajwa na chama hicho bado wako serikalini.
Alisema hatua ya watuhumiwa hao kuwa wajumbe wa vikao nyeti vya Kikatiba, kunaonyesha namna gani viongozi wa CCM wasivyo makini na kwamba, hali hiyo ndiyo inawafanya wananchi wapoteze imani na chama hicho.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, alisema hata CCM ingejivua magamba kumi na ikajichuna hadi ngozi, haiwatishi na wataendelea kupambana nao hadi wang’oke madarakani.
Alisema kimsingi Chadema kinafurahi iwapo CCM itazidi kuimarika kwani kushindana na chama dhaifu haitakuwa jambo la maana kwao.
“Mimi sioni wamejivua gamba kwa namna gani. Mabadiliko haya tunayaona kila siku. Lakini watu ni wale wale na tabia zile zile. Binafsi nafurahia mabadiliko ya CCM. Nataka tupambane na chama imara,” alisema.
Sheikh wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum, alisema sekretarieti mpya ya CCM iliyoundwa, ni timu nzuri.
Alisema anaamini inaweza kuleta mabadiliko makubwa na kurejesha heshima kwa chama hicho iliyoanza kupotea.
Sheikh Alhad alisema hayo alipozungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE jana.
“Uzoefu wao katika chama na serikali naujua. Uwajibikaji wa Mukama, ni mchapakazi sana na wote wengine,” alisema Sheikh Alhad.
Alisema jambo lingine linalompa matumaini juu ya watendaji hao wapya wa CCM, ni kutokana na kutokuwa na makundi, ambayo alisema ni tatizo kubwa lililokuwa likikitafuna chama hicho.
No comments:
Post a Comment