"Huduma itasitishwa Ijumaa Kuu yaani Aprili 22 na Jumapili ya Pasaka, Aprili 24 na itaendelea Aprili 23 na Aprili 25 baada ya Pasaka," alisema.
Mchungaji Mwasapila amewataka wagonjwa wanaopanga kwenda kupata tiba kwake wakati wa Sikukuu ya Pasaka kuangalia ratiba yake hiyo ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima.
Katika hatua nyingine, mgogoro wa mapato yanayotokana na wagonjwa wanaokwenda kupata tiba kwake, umechukua sura mpya baada ya Halmashauri ya Kijiji cha Samunge kupitisha uamuzi wa kuanza kukusanya ushuru wake mbali na kuzuiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Kijiji hicho kimesema sasa kitatoza ushuru wa Sh2,000 kwa kila gari linalofika kwa Mchungaji huyo huo ukiwa ni mbali na ule wa Sh5,000 unaotozwa na Halmashauri ya Wilaya.
Katika kikao kilichofanyika jana hapa Samunge, pia wajumbe kwa kauli moja walipinga uamuzi wa Halmashauri ya Ngorongoro na Serikali Kuu kuingilia masuala ya maendeleo ya kijiji chao bila ya kuwashirikisha.
Akitangaza uamuzi huo jana, Diwani wa Kata ya Samunge, Jackon Sandea alisema wataanza kukusanya ushuru mara tu baada ya kupata idhini ya Mkutano Mkuu wa Kijiji utakaofanyika kesho na kufuatiwa na kikao cha maendeleo Kata ya Samunge.
"Tumekubaliana halmashauri wao wakusanye hizo Sh5,000 zao na sisi tutaanza kukusanya zetu Sh2,000 kwani, Mchungaji Ambilikile yupo kijijini kwetu na sisi ndiyo tunaopata adha ya kupokea maelfu ya wageni na siyo wilayani au mkoani," alisema Sandea na kuongeza:
"Wao wameleta barua ya taarifa tu kutaka sisi tusichukue ushuru lakini, hatujawahi kukaa pamoja na kushauriana na tunaona uamuzi wao huu ni kuingilia mamlaka halali ya kijiji."
Alisema wanashangaa kuona Serikali Kuu inataka tena ipewe Sh3,000 kwa kila gari wakati tayari inakusanya fedha za ukaguzi wa magari yote yanayokwenda Samunge, na fedha za kutoa vibali.
Uamuzi huo wa kijiji kutaka kuchukua ushuru huenda ukaibua mgogoro mkubwa wakati wa kukusanya mapato kwani tangu April 6 mwaka huu, watendaji wa halmashauri hiyo walipoanza kukusanya ushuru wa Sh5,000 na kuwatimua wakusanya ushuru wa kijiji hicho.
Aomba waliokwama Bunda waruhusiwe
Katika hatua nyingine, Mchungaji Mwasapila, ameiomba Serikali kupunguza masharti kwa watu waliokwama katika Mji wa Bunda, mkoani Mara ili waweze kufika Samunge kupata tiba.
Akizungumza na Mwananchi kwa niaba ya Mchungaji Mwasapila, Msaidizi wake, Fred Nsajile alisema wamepata taarifa za mamia ya watu kuendelea kukwama wilayani Bunda kutokana na utaratibu wa kuruhusu magari kuwa mgumu.
"Mchungaji anaomba watu wanaopitia Bunda waruhusiwe kwa wingi kuliko maeneo mengine kwani eneo hilo linatumiwa na mikoa mitano na watu kutoka nje ya nchi," alisema
Jana wagonjwa wanaliozuiwa katika Kituo cha Bunda walifunga barabara kuu ya Mwanza-Musoma kwa saa kadhaa na kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria wakishinikiza kufunguliwa kwa kizuizi hicho.
Tukio hilo limetokana na jazba iliyosababishwa na kifo cha mgonjwa mwenzao, aliyefariki dunia juzi baada ya kucheleweshwa kituoni hapo kuendelea na safari.
Mgonjwa huyo mwanamume ambaye hadi sasa hajatambulika jina lake mkazi wa Kijiji cha Kakola, wilayani Kahama, Shinyanga alifariki juzi majira ya saa tisa alasiri.
Tukio hilo la kufunga barabara limekuja siku mbili tu baada ya wagonjwa hao kufanya hivyo Ijumaa iliyopita. Hata hivyo, Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Jeshi la Polisi kiliwatawanya watu hao baada ya kukaa hapo kwa takriban saa mbili.
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wagonjwa hao walisema waliamua kufanya hivyo ili kufikisha ujumbe wao kwa Serikali.
Wageni waongezeka Samunge
Foleni ya magari yanayopeleka wagonjwa kwa Mchungaji Mwasapila juzi na jana iliendelea kuongezeka na kufikia takriban kilometa 10.
Kuongezeka kwa magari kulitokana na dawa kumalizika mapema Jumamosi wiki iliyopita na kuchelewa kuanza kwa utoaji wa dawa siku ya Jumapili utoaji wa dawa ulichelewa kuanza.
Idadi ya watu kutoka nje ya nchi wanaokwenda kupata tiba Samunge imekuwa ikiongezeka sasa na wengi wanatoka nchi jirani ya Kenya na nchi za Ulaya.
Jana wageni kadhaa kutoka Uingereza waliongozwa na Colin Higgins walitua Samunge na ndege ndogo na kupata kikombe cha dawa. Higgins ambaye ni mfanyabiashara wa magari ya mafuta mkoani Morogoro, alikuwa ameambatana na Grain Mcdonald. Donald Mcdonald, Niel Mcdonald na Watanzania, Annie Voltaire na Dorothy Sen.
source mwananchi
No comments:
Post a Comment