Pages

Tuesday, April 12, 2011

Chenge, Rostam watoswa rasmi

Kama ni kujivua gamba, basi mchakato huo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ulianza jana baada ya makada wake mashuhuri, Andrew Chenge na Rostam Aziz, kuondolewa rasmi katika nafasi za ujumbe wa Kamati Kuu (CC).

Mabadiliko hayo yamefuatia kujiuzulu kwa Sekretarieti na wajumbe wa kuchaguliwa wa CC Jumamosi iliyopita ukiwa ni mkakati ulioelezwa kuwa unalenga kufanya mageuzi makubwa ndani ya CCM.

Wengine ambao walikuwa wajumbe wa Kamati Kuu iliyojiuzulu na hawakurudi katika mchujo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliyekuwa Katibu wa Ushirikiano wa Mambo ya Nje. Mwingine ni Margaret Sitta.

Katika uchaguzi uliofanyika jana wakati wa kikao cha siku mbili cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, wajumbe waliochaguliwa kuunda CC mpya kutoka Zanzibar ni: Samia Suluhu ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano); Dk. Hussein Mwinyi ambaye pia ni waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Mwanasiasa mkongwe na mbunge wa viti maalum, Dk. Maua Daftari; Mwanasiasa mkongwe na mbunge wa Uzini, Mohammed Seif Khatib; Profesa Makame Mbarawa ambaye pia ni Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Tekinolojia; Yusuf Omar Mzee ambaye pia ni Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; na Shamsi Vuai Nahodha ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani.

Waliochaguliwa kutoka Bara ni Mwanasiasa mkongwe, Abdallah Kigoda, William Lukuvi ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge; Stephen Wasira ambaye pia ni Waziri wa Nchi ofisi ya Rais na Mahusiano na Uratibu, Mwansiasa mkongwe, Abdulrahaman Kinana; Mwanasiasa mkongwe Zakia Meghji, Pindi Chana na Constantine Buhebe ambaye ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera.

Rostam ambaye ni Mbunge wa Igunga na Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi walikuwa wajumbe wa CC iliyoundwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa CCM wa mwaka 2007.

Kadhalika, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete aliwateua kuwa wajumbe wa NEC katika nafasi za upendeleo makada wanane.

Waliochaguliwa ni Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo; Emmanuel Nchimbi; Mbunge wa Bumbuli, January Makamba; Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah, muasisi wa CCM, Peter Kisumo na Haji Omar.

Wengine walioteuliwa ni Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati, Zanzibar, Juma Ali Shamhuna, Katibu Mkuu Mstaafu, Wilson Mukama na Mbunge wa Iramba Magharibi, Lameck Mwigulu Mchemba

Katika hatua nyingine, NEC imewateua baadhi ya makada wa chama hicho kuwa wajumbe wa Sekretarieti yake.

Waliochaguliwa ni Wilson Mukama (Katibu Mkuu), John Chiligati (Naibu Katibu Mkuu Bara), Vuai Ali Vuai (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar), Nape Nnauye (Uenezi na Itikadi), Lameck Mugulu Mchemba (Fedha na Uchumi) na Asha Abdallah Juma (Oganaizesheni).

Mukama anayechukua nafasi aliyokuwa anaishikilia Yusuf Makamba, aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Chiligati anayechukua nafasi iliyokuwa inashikiliwa na George Mkuchika, alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa sekretarieti iliyopita. Pia aliwahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Hivi sasa ni Mbunge wa Manyoni Mashariki.

Kabla kuchaguliwa kushika nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Ramadhan Ferouz, Vuai Ali Vuai alikuwa Katibu wa Uenezi Zanzibar.

Nape anayechukua nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Chiligati, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara.

Asha abdallah Juma ambaye ni Waziri wa zamani wa Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana Zanzibar, anachukua nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Kidawa Saleh.

Mchemba anajaza nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Mbunge wa Mvomero, Amos Makalla.

JK: MAFISADIWAJIWAJIBISHE

Hatua ya kwanza ni kuwabana watuhumiwa wawajibike wenyewe

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, amesema chama hicho kimeamua kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa wa vitendo vya utovu wa maadili.

Akifunga kikao cha NEC jana usiku mjini hapa, alisema hatua ya kwanza ni kuwabana watuhumiwa wawajibike wenyewe.

Rais Kikwete alisema hatua ya pili ni chama kuwawajibisha ikiwa watakataa kuwajibika wenyewe.

Tumekubaliana kwamba vitendo vya rushwa tunavichukia na tumeanza kuchukua hatua ili wenye kuhusishwa na vitendo vya rushwa wawajibishwe,” alisema na kuongeza:

Tumeanza safari ya kujenga upya chama chetu. Umoja wetu, mshikamano wake ndio utakaotufikisha mbele, kila mmoja atimize wajibu wake. Tumefanya maamuzi makubwa, na magumu lakini baridii.”

Alisema suala la utovu wa maadili ni miongoni mwa mambo ambayo yamekirudisha nyuma chama.

Hata hivyo, alisema hakuna moto uliowaka katika ukumbi wa mkutano na wajumbe walitoka bila unyonge na hakuna wa kumtumia mwenzake ujumbe fulani kwamba alimtukana.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungwa kwa kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Chiligati, alisema baada ya miezi mitatu wanachama ambao wanatajwa katika kashfa mbalimbali kama Richmond, Dowans EPA, Kagoda wawajibike.

Alisema hata kama hakuna ushahidi inatosha kwa chama kuwawajibisha.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment