Baraza la Madiwani Jiji la Arusha limepitisha bajeti ya zaidi ya Sh. bilioni 48.1 kwa mwaka huu wa fedha wa 2011/ 2012, licha ya madiwani 11 wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) kususia kikao hicho kilichofanyika jana kwa kutoka ukumbini.
Baraza hilo likiwa na wajumbe 16 kutoka vyama vya CCM na TLP, lililazimika kuendelea na kikao na kupitisha bajeti hiyo, huku baadhi ya wajumbe wa baraza hilo kutoka vyama hivyo viwili wakishutumu hatua ya madiwani wa Chadema kususia kikao hicho.
Awali, baada ya wajumbe wote kuingia katika ukumbi, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Estomiah Chang’a, alitoa taarifa ya idadi ya madiwani waliokuwa ukumbini wakiwemo wa Chadema, CCM na TLP kuwa ni 25.
Alisema idadi hiyo ni zaidi ya akidi ya theluthi mbili ya wajumbe wote 32 wanaotakiwa kuhudhuria kikao hicho.
Lakini wakati Meya wa Jiji la Arusha, Mstahiki Gaudence Lyimo, aliposimama kwa ajili ya kufungua kikao hicho, madiwani wa Chadema wakiongozwa na John Bayo wa kata ya Elerai walinyanyuka vitini na kutoka nje ya ukumbi.
Hata hivyo, Chang’a, alisema kanuni na taratibu zinaelekeza kwamba iwapo mjumbe yeyote wa kuchaguliwa atapata wito na akaitikia na kufika ukumbini ni dhahiri mjumbe huyo atakuwa amehudhuria kikao hicho na hivyo kuchangia kufikia idadi ya wajumbe wanaotakiwa kufikisha akidi ya kikao ya theluthi mbili hata kama atakuwa ameondoka ukumbini.
Mbali na wadiwani wa Chadema kuingia ukumbini na kujiorodhesha katika kitabu cha mahudhurio, Bayo, aliamua kuchukuwa rejesta ya majina na kukatakata majina yao.
Akizungumza mara baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Diwani wa TLP kutoka kata ya Sokoni One, Maiko Kivuyo, alisema wamepitisha bajeti ya jiji kwa manufaa ya wananchi wa Arusha.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment