WABUNGE wa Kambi ya Upinzani wameupinga Muswada wa Sheria ya Wafamasia ya mwaka 2010 na kutaka urejeshwe katika Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ili ufanyiwe marekebisho zaidi.
Muswada huo uliowasilishwa bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, umeonekana kupingwa waziwazi na wabunge kutokana na mapendekezo yaliyomo ndani yake kuonekana kuwa na mapungufu. Muswada huo pamoja na mambo mengine unakusudia kuweka masharti ya kudhibiti na kusimamia taaluma na maadili ya wafamasia katika utoaji wa huduma huku ukilenga kuhamisha nguvu za Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi (TFDA) na kuzipeleka katika Baraza la Famasi.
Muswada huo uliosomwa kwa mara ya pili, unakusudia kufuta sheria namba moja ya mwaka 2003 ya mamlaka hiyo ili kuhamisha masharti yanayohusiana na taaluma ya famasi ambayo chini ya sheria hiyo yalikuwa yakisimamiwa na TFDA.
Chini ya muswada huo, Baraza la Famasi linapewa mamlaka ya kudhibiti na kusimamia taaluma na maadili ya wafamasia sambamba na usimamizi wa biashara ya dawa hususan utoaji wa leseni.
Aidha, wamelitaka Baraza la Famasi libaki na kazi ya kudhibiti na kusimamia taaluma na maadili ya wafamasia na suala la biashara libaki chini ya usimamizi wa TFDA.
Maoni ya kambi ya upinzani yaliyotolewa na msemaji wa wizara hiyo, Dk. Gervase Mbassa, yaliweka wazi kuhusu msimamo wa kambi dhidi ya muswada huo.
“Muswada huu unataka kuweka utaratibu wa kusimamia taaluma na biashara ya famasi. Kambi ya upinzani inataka maelezo ya kina kabisa kwamba ni kwanini chombo cha kitaaluma kiwe chombo cha kusimamia biashara.
“Kambi ya upinzani ina shaka na muswada huu. Ni dhahiri huu muswada haujafanyiwa tafakuri ya kutosha na ni kama vile unataka kuridhisha kikundi kimoja katika jamii.
“Ni vema muswada huu urejeshwe kwenye kamati ili ukafanyiwe mabadiliko muhimu ya kuondoa vipengele vyote vinavyohusu usimamizi wa biashara ya famasi ili kutenganisha biashara na taaluma,” alisema Dk. Mbassa.
Akitilia nguvu hoja hiyo, Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Kabwe Zitto, alitaka kifungu cha nne cha muswada huo kiondolewe chote au muswada huo urejeshwe kwenye kamati.
“Baraza la Famasi libaki na kazi ya kusimamia taaluma na maadili tu halafu kazi ya kusimamia biashara waachiwe TFDA, huu muswada unafilisi majukumu ya TFDA ambayo hivi sasa ina uzoefu wa kutosha tangu mwaka 2003, iweje leo wapokonywe nguvu na Baraza?” alihoji Kabwe.
Naye Mbunge wa Vunjo Agustino Mrema (TLP) akichangia muswada huo alisema malengo ya muswada huo ni mazuri kwa kuwa pamoja na mambo mengine unalenga kudhibiti tatizo la wafamasia bandia.
Akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii kwa niaba ya Mwenyekiti, Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile (CCM), alisema kamati yake imeridhishwa na muswada huo.
“Kamati inaunga mkono hatua ya serikali ya kuleta muswada huu kwa lengo la kuwa na Baraza la Famasi, ambalo litakuwa na jukumu la kusimamia taaluma katika fani ya famasia.
“Pamoja na majibu ya waziri, kamati iliendelea kushauri kwamba kifungu cha 37 (1) (b) kiangaliwe upya, ili jukumu la utoaji wa leseni za uingizaji wa dawa na utengenezaji wa dawa nchini libaki kuwa la TFDA,” alisema Dk. Ndugulile
SOURCE TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment