KAMATI ya Bunge ya Miundombinu, imeikataa Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi hadi serikali itakapowasilisha kiasi cha Sh113 bilioni za bajeti ya mwaka wa fedha unaoisha Juni 31, mwaka huu. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Serukamba alisema serikali haikuwasilisha fedha zote zilizoombwa na wizara hiyo ambazo zilikuwa ni Sh95 bilioni na badala yake iliwasilisha Sh45 bilioni hadi Machi, mwaka huu.
Alisema wahisani walitoa Sh65 bilioni katika bajeti hiyo lakini hadi Machi, mwaka huu ni Sh2bilioni tu ambazo zilikuwa zimewasilishwa katika wizara hiyo. Alisema fedha hizo zingetosha kuboresha miundombinu nchini ikiwamo barabara (kwa kiwango cha lami) viwanja vya ndege na reli. “Yaani inachekesha kwa kweli, leo tunapitisha Bajeti ya Serikali wakati iliyopita pesa haikufika kama ilivyotakiwa! Sasa tunapitisha bajeti ya nini? Lazima ikwame tutakutana huko Bungeni zitolewe ufafanuzi hizi pesa,” alisema Serukamba.
Mwenyekiti huyo alisema ili bajeti hiyo ipite ni lazima serikali itoe fedha za kufufua miundombinu kwanza ambazo ni pamoja na Sh1.6 bilioni kwa ajili ya kuboresha usafiri wa meli, Sh23 bilioni kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Sh 241 bilioni ziende Shirika la Reli Tanzania (TRL).
Serukamba ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), alisema serikali haiko makini kwa sababu haitoi kipaumbele kwa bajeti ya uchukuzi. Alisema nchi yoyote yenye maendeleo duniani lazima itoe kipeumbele katika miundombinu ili ifanye kazi ya kusafirishia bidhaa mbalimbali za kukuza uchumi. “Hakuna nchi yenye maendeleo ambayo haina barabara, reli, anga, bandari za uhakika za kusafirishia mazao na mengineyo kwa ajili ya uchumi wa nchi.”
Alisema mapendekezo ya bajeti hiyo ambayo yaliwasilishwa mbele ya kamati yake kwa mwaka 2011/2012, ilikuwa na upungufu hivyo kulikuwa hakuna sababu za kuipitisha. Alisema serikali ina fedha za kutosha lakini akashangaa kuona ATCL linakufa huku likiwa linaangaliwa kama ilivyo kwa TRL ambalo nalo linasuasua. Serukamba alimwambia Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu kuwa serikali inatakiwa kujipanga tena kwa makini kuliokoa taifa kiuchumi. Alisema inawezekana wizara hiyo ikawa na malengo mengi mazuri lakini yakakwamishwa na bajeti inayopatiwa na Hazina.
“Sitashangaa kwani leo tumemsikia waziri hapa akieleza malengo mengi ambayo wanataraji kuyafanya lakini sasa watayafanyaje ikiwa hakuna fedha za kutosha," alisema. Awali, Waziri Nundu alisema katika jitihada za kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, wizara yake kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), imeendelea kuhimiza matumizi ya mabasi makubwa tu kutoa huduma katikati ya jiji, hatua ambayo kwa kiasi kikubwa imepunguza tatizo. Wabunge wahoji hatima ya ATCL
Wabunge wa Kamati hiyo walitaka kujua hatima ya ATCL wakisema licha ya kutofanya kazi, bado wafanyakazi wake wanalipwa mishahara. Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali aliitaka serikali kueleza wafanyakazi hao watalipwa mishahara mpaka lini wakati shirika lenyewe halifanyi kazi kwa muda mrefu sasa.
Alisema ingekuwa vizuri Waziri Nundu aeleze kiundani suala la wafanyakazi hao kulipwa mishahara na inakotoka. Pia alitaka kujua ni lini serikali italifufua tena shirika hilo kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa nchi ambao umeshuka kwa kasi baada ya kufa kwake.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohamed Mnyaa alisema ni vigumu kusikia wafanyakazi wanalipwa mishahara mpaka leo wakati shirika lenyewe limeshakufa. Akijibu hoja hiyo Waziri Nundu alisema katika jitihada za kuinusuru ATCL, serikali imekuwa ikilipa mishahara ya wafanyakazi na fedha za matengenezo ya ndege. Alisema serikali bado ipo katika jitihada za kulifufua shirika hilo ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na wawekezaji mbalimbali.
No comments:
Post a Comment