Pages

Wednesday, March 2, 2011

Waziri Sitta arusha tena kombora Serikalini

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema hasara ambazo taifa limepata kutokana na mikataba mibovu ni matokeo ya kasoro zilizopo katika mfumo wa utoaji wa elimu nchini.Sitta alisema hayo juzi usiku kwenye Sherehe za Maadhimisho ya miaka 10 ya Shirika la HakiElimu zilizofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema kasoro hizo zimesababisha mfumo huo wa elimu nchini kuzalisha watendaji mafisadi, wasiokuwa na maadili katika utendaji.Sitta alisema sekta ya elimu ni kama imepewa kisogo, kiasi kwamba hakuna uwiano wa kiutendaji wa watu wanaohitimu mafunzo mbalimbali ikilinganishwa na vyeti vyao vinavyoonyesha kwamba walifanya vizuri darasani."Tumeshuhudia miaka 10 iliyopita, serikali imeingia hasara kutokana na baadhi ya viongozi kukosa uadilifu, wakaliingizia hasara taifa kwa kusaini mikataba feki," alisema Sitta na kuongeza:"... Hayo yote ni kwa sababu ya kuipa kisogo sekta ya elimu. Hii inatoa viongozi wasiojiamini na wanaokosa maadili." Hii ni mara ya pili kwa Sitta kuikosoa serikali ambayo yeye ni mmoja wa mawaziri wake. Moja ya mambo ambayo Sitta amewahi kuipingana na serikali ni malipo ya fidia kwa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans Tanzania Ltd.Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), alitaka serikali isiilipe fidia ya Sh94 bilioni kwa kampuni hiyo akieleza kuwa kufanya hivyo ni sawa na kuhujumu uchumi wa nchi.

Katika hotuba yake juzi, Sitta alisema serikali inawajibika kuhakikisha inawekeza katika sekta ya elimu ili kuwaandaa viongozi wenye nidhamu na maadili."Tunataka viongozi wajiamini wakiwa kazini na waweze kutetea maslahi ya nchi, vinginevyo nchi itaendelea kuzalisha viongozi wajanja wajanja na wahuni tu," alisema. Waziri Sitta alitaka Shirika la HakiElimu kuendelea kusema ukweli na kufichua mambo yanayodidimiza elimu kwa maslahi ya watu wachache wenye nia mbaya.Alisema kwa bahati nzuri kwa sasa yupo serikalini na kuahidi kuwa balozi wa HakiElimu na kuwatetea pale watakapobezwa na kutishwa na baadhi ya watu wenye nia mbaya wanapoeleza ukweli.“Napenda kuwaambia kwamba nitakuwa balozi wenu na kuwaunga mkono na nitaendelea kuwa pamoja na nyie hadi tuhakikishe tunaleta maendeleo katika sekta ya elimu mchango wenu ni mkubwa sana,”alisema Sitta.Serikali ya Awamu ya Tatu ilitishia kuifungia HakiElimu na kuionya kuacha kutumia matangazo yake katika vyombo vya habari, kueneza chuki miongoni mwa watoto na vijana nchini. Matangazo ya HakiElimu ambayo yaliiudhi serikali ni pamoja na lile serikali kueleza kuwa uchumi unapanda wakati hali ya wananchi bado duni. Jingine ni lile lililoonyesha matatizo sugu ya walimu wanaofanyia kazi maeneo ya vijijini. Tangazo hilo lilimuonyesha mwalimu akitumia siku mbili kufuata mshahara mjini.

Akitumia baskeli lakini anapofika benki anakuta mshahara bado haujaingizwa.Waziri Sitta ambaye alikuwa Spika katika Bunge la Tisa, alisema kila mtu anatambua mchango na umuhimu wa HakiElimu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001, hivyo hakuna haja ya shirika hilo kuogopa kusema ukweli katika harakati za kuboresha elimu nchini.“Ukweli ni kwamba katika nchi zilizoridhia makubaliano ya Dira ya Elimu ya mwaka 2015 na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki tuna nchi tano, lakini Tanzania ni ya mwisho kielimu. Hali hii inatishia uhai wa nchi,” alisema Sitta.Alisema kuwa elimu bora inaweza kumbadili mtu kitabia na kiuchumi na hivyo kumfanya ajiamini.Hata hivyo, Waziri Sitta alisema tofauti na ukweli huo, sasa umaskini hasa kwa watu wa hali ya chini nchini, unazidi kuongezeka huku baadhi ya viongozi wasiokuwa na maadili wakiendelea kulipeleka taifa kusikokuwa na mwelekeo. Waziri Sitta alifafanua kuwa mtu hapimwi kwa ufaulu wa mitihani na shahada alizonazo, bali anapimwa kutokana na utendaji wake na maadili mema kazini na kuwa mstari wa mbele katika kulinda maslahi ya taifa.“Kiongozi hapimwi kwa shahada, vyeti wala kiwango cha ufaulu wa mitihani yake, maana Tanzania ina viongozi wengi wenye shahada na vyeti kibao, lakini wanayofanya viongozi hao wenye shahada, wote tunayajua,” alisema.Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya HakiElimu Joaquine De-Mello alisema hadi wanapoadhimisha miaka hiyo kumi tangu kuanzishwa kwa shirika hilo, Hakielimu imepitia changamoto nyingi ikiwamo vitisho wanapojaribu kueleza ukweli.“Tumepitia milima na mabonde maana siku zote mtu anayeeleza ukweli anaonekana ni mchochezi, lakini baadhi ya watu wametambua mchango wa HakiElimu na baadhi yao hadi sasa hawatambui mchango wetu katika harakati za kuleta maendeleo ya elimu nchini,” alisema De-Mello.


Alizitaja changamoto nyingine inazoikabili HakiElimu kuwa ni upatikanaji wa taarifa katika taasisi zinazosimamiwa na serikali.Alisema baadhi ya watendaji katika taasisi hizo, hawataki kueleza ukweli wakidhani HakiElimu inataka kupotosha jamii."Sisi lengo letu siyo kupotosha, tunataka kuielimisha jamii na kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu na wanafunzi kupata elimu yenye manufaa na kumwezesha kujiajiri na kuajiriwa," alisema.De-Mello alitaja kikwazo kingine cha maendeleo ya elimu nchini kuwa ni baadhi ya viongozi kutaka kuchanganya elimu na siasa…"Hii ni hatari katika maendeleo ya elimu ambayo ndiyo mhimili wa kila jambo duniani."

No comments:

Post a Comment