Waandishi wa habari walifika hapo jana na kukuta shule hiyo yenye wanafunzi 269 na walimu saba wa kuanzia chekechekea, darasa la kwanza hadi la saba ikiwa na vyumba vinne pekee vya madarasa.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Jonathan Chengula aliwaambia waandishi wa habari kuwa katika shule hiyo iliyoanza na kusajiliwa mwaka 2003, wanafunzi wa darasa la kwanza wanasoma chumba kimoja kwa wakati mmoja na wale wa chekechea, darasa la pili wanasoma pamoja na wenzao wa darasa la tatu, la sita na la tano, huku wale wa darasa la saba wakitumia chumba kimoja na wa darasa la nne.
“Tatizo kubwa ambalo linatusumbua katika shule yetu ni upungufu wa madarasa. Tuna madarasa manne tu hivyo imetulazimu kuweka mbao za kufundishia mbili katika chumba kimoja ili madarasa mawili yaweze kutumia kwa wakati mmoja,” alisema.
Kwa mujibu wa mwalimu mkuu huyo, ili kukabiliana na upungufu huo wa madarasa na kutokana na mazingira ya shule hiyo, ndiyo maana wameramua wanafunzi wa madarasa mawili tofauti wasome katika chumba kimoja kwa kugeuziana migongo kwa maana ya kuwa wengine wanageukia upande wa kulia na wengine kushoto.
“Kama mnavyowaona hawa waliogeukia huko ni darasa la saba na hawa wengine ni darasa la nne na katika darasa hili jingine wanasoma darasa la pili na tatu ndivyo tunavyo kwenda," alisema.Alisema kuwa mwalimu wa darasa la saba anapoingia kufundisha, wa darasa la nne anasubiri mwenzake amalize huku wanafunzi hao wa darasa la nne wakiwemo humo humo ndani wakisikiliza wale wa darasa la saba wanavyofundishwa.
Alisema wakati mwingine walimu huamua kuwatoa nje na kuwaweka chini ya mti kama umefika wakati wa kusoma kitabu cha Kiswahili ili wasome wakiwa nje na wengine waendelee na masomo.
Mwalimu aliyekuwa darasani akifundisha, Shufaa Ramadhani alisema mazingira hayo ya ufundishaji ni magumu kwani kuna athari kubwa kwa wanafunzi na upande wa mwalimu kwani kufundisha wote kwa pamoja pia ni vigumu.
Alisema kuwa utaratibu huo unawaathiri watoto kisaikolojia kwani kuna uwezekano wa kusahau yale ambayo wamefundishwa na mwalimu wao na badala yake kusikia ya upande wa pili ambayo ni masomo ya darasa jingine ambalo tayari walishayapitia au bado hawajapitia.
Mwalimu Shufaa alisema walimu wanaathirika kwa kupoteza vipindi vingine kwa mujibu wa uandaaji wa masomo na vipindi kwani inamlazimu asubiri mwenzake amalize kufundisha na ndipo aingie na kufundisha somo lake.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, George Kagomba hakupatikana kuzungumzia tatizo hilo na alipotafutwa kwa simu alijibu kuwa yuko kwenye kikao cha maandalizi ya Mbio za Mwenge.
Mkurugenzi huyo aliwataka waandishi kwenda kwa Ofisa Elimu wa Wilaya ya Mbarali. Hata hivyo, aliyekuwa akikaimu ofisi hiyo hakuwepo. Ofisa elimu wa Wilaya alikuwa amesafiri kikazi.
SOURCE MWANANCHI
No comments:
Post a Comment